2 Thessalonians 3

Hitaji La Maombi

1 aHatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu. 2 bOmbeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini. 3 cLakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. 4 dNasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. 5 eBwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Al-Masihi.

Onyo Dhidi Ya Uvivu

6 fNdugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Isa Al-Masihi, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. 7 gMaana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8 hwala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. 9 iTulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo. 10 jKwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”

11 kKwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12 lBasi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Isa Al-Masihi, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe. 13 mKwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.

14 nIkiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu. 15 oLakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Salamu Za Mwisho

16 pBasi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

17 qMimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.

18 rNeema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe nanyi nyote. Amen.
Copyright information for SwhKC